Duniani kote, lakini hasa Marekani, watu wanaonekana kuthamini sana kujitegemea bila kuwategemea wengine. Watu wanaoonyesha sifa hii hujipambania maishani, bila kuomba wala kutarajia chochote kutoka kwa wengine.
Nadhani wazo hili linatokana na walowezi wa mwanzo. Hawa walikuwa wanaume na wanawake waliosafiri kwa miguu kupitia nchi mbalimbali mpya wakitafuta mahali pa kutulia na kupaita nyumbani. Kulikuwa na maduka machache ya bidhaa za matumizi ya jumla, nao waliishi kwa kujitegemea kadiri walivyoweza.
Ingawa hali hii inaweza kuonekana kuonyesha nguvu, ukweli ni tofauti kwa kiasi fulani siku hizi. Siku hizi watu wanatumia teknolojia kujizungushia kwa makusudi mazingira ya kujitenga.
Wazee wengi wamejikuta wakizidi kutengwa na marafiki na familia. Bila shaka COVID ilizidisha hali hii, lakini mbegu za kujitenga huku zilikuwa zimepandwa muda mrefu kabla COVID haijasikika kamwe.
Kujitenga si Hali ya Kiasili
Tukitazama nyuma hadi Bustani ya Edeni, tunaona kwamba Adamu aliumbwa kabla ya Hawa. Ingawa kulikuwa na wanyama wengi, Adamu hakuwa na mwenzi wa kweli. Naye BWANA Mungu akasema, Si vema mtu awe peke yake; nitamfanyia msaidizi anayemfaa … Naye Adamu akawapa majina ng’ombe wote, na ndege wa angani, na kila mnyama wa porini; lakini kwa Adamu hakupatikana msaidizi anayemfaa –Mwanzo 2:18-20.
Naye BWANA Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; akachukua ubavu wake mmoja, akapafunika mahali pake kwa nyama; na ule ubavu ambao BWANA Mungu alikuwa ameutwaa kutoka kwa mwanamume akaufanya mwanamke, akamleta kwa mwanamume –Mwanzo 2:21-22. Bila shaka, huu ulikuwa mwanzo wa ndoa, lakini jambo muhimu zaidi la kuona hapa ni kwamba si hali ya kawaida kwa wanadamu kuwa peke yao. Tunatamani kuwa na wenzi, na si kuwa tu na mbwa au paka wa kufugwa.
Kujitenga Kunaweza Kusababisha Kukata Tamaa
Pengine hakuna simulizi linaloonyesha kwa uwazi hatari za kujitenga kama simulizi la Eliya. Tunajua kutoka kitabu cha Biblia cha 1 Wafalme kwamba Eliya alikuwa nabii wa Mungu mwenye ari kubwa.
Alileta ujumbe kutoka kwa Mungu kwa Ahabu kwamba hakutakuwa na mvua, na kulikuwa na ukame mkali kwa miaka mitatu na nusu iliyofuata. Wakati huo, Eliya alikaa jangwani na kisha akaishi na mjane huko Sarefathi.
Wakati wote huo, alilishwa kimiujiza kwa nguvu za Mungu, kwanza na kunguru na kisha kupitia unga na mafuta ambayo Mungu alimpatia mjane aliyeishi naye. Kwa nguvu za Mungu, alimfufua mwana wa mjane.
Kisha ukafika wakati alipowapa manabii wa Baali changamoto ya kushindana naye kwenye Mlima Karmeli, akapata ushindi wa wazi kwa ajili ya Mungu. Moto wa kimiujiza ulishuka kutoka mbinguni kujibu sala yake. Kweli, Mungu alikuwa akifanya mambo makubwa katika maisha yake.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye, Eliya alikuwa akikimbilia jangwani kuokoa maisha yake. Yezebeli alikuwa ametishia kumuua, na badala ya kumtumaini Mungu, alikimbilia Mlima Horebu ambako aliisikia sauti ya Mungu.
Mungu alipomwuliza alikuwa anafanya nini pale, Eliya akajibu, …Nimekuwa na wivu mwingi kwa ajili ya BWANA Mungu wa majeshi: kwa maana wana wa Israeli wameliacha agano lako, wamezibomoa madhabahu zako, na wamewaua manabii wako kwa upanga; nami, mimi peke yangu, nimebaki; nao wanatafuta kuniua –1 Wafalme 19:10.
Tunaweza kuona hapa sababu kubwa ya udhaifu wa Eliya. Alihisi kuwa peke yake kabisa. Mungu aliisahihisha dhana potovu ya Eliya aliposema: Lakini nimejibakizia watu elfu saba katika Israeli, magoti yote ambayo hayajampigia Baali magoti, na kila kinywa ambacho hakijambusu –1 Wafalme 19:18.
Kuwepo kwa wanaume na wanawake hao katika Israeli hakukumsaidia Eliya sana kwa kuwa hakukaa nao. Kujitenga kwa Eliya kulimfikisha kwenye udhaifu na kukata tamaa.
Simulizi la Paulo pia linakuja akilini. Mtume Paulo alikuwa mtu aliyeonekana kuwa na nguvu karibu zisizo na kikomo na bidii isiyozimika kwa mambo ya Mungu, lakini barua yake ya mwisho kwa Timotheo akiwa gerezani ilimfunua mtu aliyehisi upweke mkubwa. Jitahidi kuja kwangu upesi: kwa maana Dema ameniacha, kwa sababu ameupenda ulimwengu huu wa sasa, naye ameenda Thesalonike; Kreske ameenda Galatia, na Tito Dalmatia. Luka peke yake yuko pamoja nami. Mchukue Marko, umlete pamoja nawe… –2 Timotheo 4:9-11.
Mtume hakuwa ameachwa. Isipokuwa Dema, wengine hawakuwa wamekimbia kwa kuogopa au kuonea aibu kufungwa kwake gerezani. Alikuwa amewatuma marafiki zake wengi kuliimarisha kanisa katika sehemu mbalimbali za Dola la Kirumi. Hata hivyo, Paulo bado alihisi kutengwa na alihitaji ndugu wema wa Kikristo, Timotheo na Marko, waje wamtie moyo alipokuwa akikabili kifo cha kishahidi.
Kujitenga Kunadhuru Afya ya Mwili
Tafiti zimeonyesha kwamba kujitenga kunahusishwa na viwango vya juu zaidi vya shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, wasiwasi, na unyogovu. Wazee waliojitenga mara nyingi huonyesha dalili za kupungua kwa uwezo wa akili, na hali yao ya kupoteza uwezo wa kiakili kutokana na demensia inaweza kuzidi kuwa mbaya.
Mara nyingi, watu wanapozeeka, hufiwa na wapendwa wao. Kufiwa na mwenzi wa ndoa kunaweza kuwafanya wazee wajitenge na wengine na wapate upweke na utengano. Hali hii nayo mara nyingi husababisha mchakato wa kuzeeka kwenda kwa kasi zaidi.
Sayansi haielewi jambo hili kikamilifu, lakini upweke husababisha kuongezeka kwa uchochezi mwilini na kudhoofika kwa utendaji wa mfumo wa kinga. Hali hii nayo inaweza kuwafanya watu wenye upweke wapate maambukizi makali zaidi na kuwa na shida ya kupata nafuu baada ya maambukizi hayo.
Ingawa tunafikiria matatizo haya kuwa yanawaathiri hasa wazee, yanaweza pia kuwaathiri watu wenye umri mdogo. Kwa watu wenye umri mdogo, mara nyingi upweke hausababishi matatizo ya kumbukumbu, lakini kwa hakika unaweza kusababisha mambo kama unyogovu, na unaweza kuzidisha sana magonjwa sugu ya uchochezi.
Kinyume cha Kujitenga
Wakiulizwa kinyume cha kujitenga ni nini, watu wengi huenda wakajibu “Kuwa na wenzi” au labda hata “Urafiki”. Kuna neno jingine lenye maana inayohusiana na Ukristo ambalo linafaa hata zaidi. Neno hilo ni ushirika.
Neno la Kigiriki lililotafsiriwa ushirika katika Agano Jipya ni “Koinonia”, na katika Biblia linazungumzia mahusiano yaliyojengwa juu ya upendo wa pamoja kwa Mungu na kwa kanisa—umoja wa imani na matamanio. Ushirika wa Kikristo unajumuisha mambo kama kusali pamoja, kutiana moyo, na hata kuteseka pamoja.
Nina wasiwasi kwamba wengi leo wanajikuta katika mojawapo ya hali mbili hatari. Kwanza, huenda si washiriki wa kusanyiko lolote la kanisa. Ingawa hali hii inaweza kuwa isiyoepukika katika mazingira fulani ya huduma za umisheni, si hali bora, na kwa hakika haipaswi kuwa hali ya kawaida. Angalau inaweza kuleta hisia ya kutengwa, na katika hali mbaya zaidi inazuia kutekelezwa kwa vifungu vingi vya Biblia vinavyohusu kutendeana mambo “ninyi kwa ninyi”. Tunahitaji ushirika, ili tutiwe moyo na pia tuwajibishwe.
Hali ya pili hatari ni kwamba waumini wengi, ingawa ni washiriki wa kanisa, hujitenga ndani ya kanisa hilo. Ukiwa mshiriki wa kusanyiko kubwa la kanisa, ni rahisi kuwa tu sehemu ya umati bila kujenga mahusiano na wengine. Hii inadhuru sawa na kutokuwa mshiriki wa kusanyiko la kanisa. Watu wengi mno huhisi upweke, hata wakiwa wamezungukwa na watu wengi.
Maandiko yanaweka wazi kwamba tunahitaji kusanyiko la kanisa. Tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tutiane moyo: na kufanya hivyo zaidi kadiri mnavyoiona siku ile ikikaribia –Waebrania 10:25.
Kuna watu wengi ambao maisha yao yamejaa marafiki na watu wanaofahamiana nao, lakini ikiwa hawana mahali pa kupata ushirika, wanakosa jambo muhimu.
Ninapowaona watu katika ofisi yangu wanaopambana na unyogovu, kuna mambo mawili ninayowaambia daima wajifanyie.
La kwanza ni kuanza kufanya mazoezi. Tafiti kadhaa zimelinganisha mazoezi na dawa za kutibu unyogovu na kubaini kwamba mazoezi yalikuwa na ufanisi sawa na dawa nyingi za unyogovu zinazoagizwa kwa kawaida. Si lazima yawe mazoezi makali sana, lakini yanahitaji kuwa ya aerobiki (ya kutosha kuongeza kasi ya mapigo ya moyo) na yafanywe kwa ukawaida.
Jambo la pili ni kushiriki kikamilifu katika kusanyiko la kanisa; haitoshi kuhudhuria tu kanisa. Kuwa na ndugu na dada wa kumwombea mtu anayepambana na matatizo, kusikiliza hali zinazomkatisha moyo, na kumtia moyo kutembea na Mungu kwa uchangamfu zaidi kunasaidia sana.
Kwa bahati mbaya, mtu anapopambana na unyogovu, jambo la mwisho analoonekana kutaka kufanya ni kujitahidi kuwa pamoja na watu wengine. Ingawa kutofanya juhudi hiyo kunaendana na hisia zake, kunazuia kutatuliwa kwa tatizo hilo.
Tunapolitafakari hili, linapaswa kutuchochea kuwafikia wale tunaowajua wanahangaika na hali ya kutengwa.
Mtu anapofiwa na mwenzi wa ndoa, mara nyingi hutiwa moyo sana katika wiki kadhaa za kwanza, lakini tunahitaji kuhakikisha kwamba katika miezi inayofuata bado kuna watu wanaoshiriki kikamilifu katika maisha yake.
Kwa maana kila mtu ataubeba mzigo wake mwenyewe –Wagalatia 6:5, haipaswi kutupa kisingizio cha kutotii amri ya Mungu ya Chukulianeni mizigo, na hivyo mtimize sheria ya Kristo –Wagalatia 6:2. Familia ya Mungu haijawekewa kikomo cha muda cha kubeba mizigo. Kuna agizo tu kwamba tunapomwona ndugu au dada yetu akihangaika, tunapaswa kumsaidia kadiri tuwezavyo.
Baraka ni kwamba siku moja, tutakapokuwa tunahangaika, tutakuwa na wanaume na wanawake wa imani wanaotuzunguka ili kututia moyo na kutuombea. Hatuwezi kubeba mizigo hii peke yetu. Pamoja, tutaufikia Mji wa Mbinguni.
Kujitenga hutokana na sababu nyingi. Wakati mwingine huonekana kuwa mtindo wa maisha uliochaguliwa, kama ilivyo mwelekeo wa asili wa watu wasiochangamana sana na wengine. Wakati mwingine mtu hulazimishwa kuingia katika hali hiyo kwa sababu ya kufiwa na wapendwa au kupata hasara nyingine kubwa. Vyovyote iwavyo, si hali yenye afya ya kuishi ndani yake.
Tunapojikuta katika hali hizi, tunahitaji kuchukua hatua ya kutafuta ushirika. Familia ya Mungu iko kwa ajili yetu ikiwa tu tutachukua hatua ya kuiendea.
Tunapowaona wengine wakihangaika, tunahitaji kuwanyoshea mkono wa kuume wa ushirika. Tunapofanya hivyo, huenda kupitia jitihada zetu ndogo tukamsaidia mtu kihisia, kimwili, na kiroho, kwa kuwa tu rafiki wakati wa kutengwa.
Viungo:
https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC2841310/
https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/29792097/
https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/23749730/
https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC5430071/



