Wimbo huu wa ibada kwa ujumla unaaminika kuwa mojawapo ya nyimbo za ibada zinazopendwa zaidi zilizotungwa katika sehemu ya mwisho ya karne ya 19. Uandishi wa maneno haya yenye kina na yaliyotungwa kwa ustadi unashangaza hata zaidi tukizingatia kwamba mwandishi wake alikuwa karibu kipofu kabisa na anaelezea uandishi wa wimbo huu kama “tunda la mateso mengi ya akili,” na “kazi niliyoikamilisha kwa muda mfupi zaidi kuliko kazi nyingine yoyote maishani mwangu.”
George Matheson, aliyezaliwa Glasgow, Scotland, Machi 27, 1842, alikuwa na uwezo mdogo wa kuona akiwa mtoto, na, baada ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Glasgow, uwezo wake wa kuona uliendelea kudhoofika kwa haraka. Isipokuwa kwa “nyakati za kuona hafifihafifi,” alikuwa kipofu kabisa kufikia umri wa miaka 18. Hali hii ya upofu ilionekana kuwa janga kwa kuwa alikuwa mwanafunzi mwenye hamu na ari kubwa ya kujifunza, lakini ilimfanya amtumaini Bwana, na iliimarisha mwenendo wake pamoja na Mungu.
Alijiunga na chuo kikuu akiwa na umri mdogo wa miaka 15 na alihitimu kwa heshima kubwa mwaka 1861 akiwa na umri wa miaka 19. Alikuwa mwanafunzi mwenye akili sana; hata alitumia miaka mingine minne baada ya kuhitimu akiendelea na masomo ya theolojia, akiwa wakati wote hajaoa. Baada ya kuhitimu alitegemea kabisa wengine, akiwategemea sana dada zake wawili, ambao walijitolea sana kiasi cha kujifunza Kilatini, Kigiriki, na Kiebrania kwa sababu walifikiri kwamba hilo lingeweza kumsaidia katika masomo yake ya theolojia. Mmoja wao aliendelea kuwa mfanyakazi mwenzake mwaminifu na msaidizi maisha yake yote, akimsaidia katika wito wake wa kuwa mchungaji na majukumu mengine ya huduma.
Baada ya kumaliza kozi yake ya theolojia, akawa mchungaji msaidizi wa Dkt. Macduff maarufu, ambaye katika kanisa lake lenye maelfu ya washiriki alikuwa amelelewa. Hata hivyo, muda mfupi baadaye, alichaguliwa kuwa mchungaji wa Kanisa la Scotland huko Innellan, mji wenye bandari na mahali pa mapumziko wakati wa kiangazi. Hapa alikaa kwa miaka kumi na nane. Familia nyingi zilikuja kutumia majira ya kiangazi hapo hasa kutiwa moyo na huduma yake ya kuhubiri.
Kila alipohubiri, Biblia iliyofunguliwa ilikuwa mbele yake alipokuwa amesimama mimbarini, na kwa waumini, alionekana kuwa akiisoma. Wakati wa mahubiri, macho yake yalitazama moja kwa moja waumini, na wengi waliondoka bila kujua kwamba walikuwa wamemsikiliza mhubiri kipofu. Ilikuwa katika kipindi hiki alipojizoeza kukariri mahubiri yake, pamoja na vifungu vya Maandiko alivyotumia katika ujumbe wake. Kumbukumbu yake ilikuwa nzuri sana kiasi kwamba mtu akimsomea mojawapo ya mahubiri yake aliyotayarisha mara mbili, au kitu kingine chochote alichotaka kukariri, angeweza tangu hapo kukirudia kikamilifu. Hata hivyo, Jumapili moja, baada ya kufanya hivi kwa miaka 12, akiwa katikati ya mahubiri yenye nguvu, kumbukumbu yake ilishindwa kabisa kufanya kazi, na mada aliyokuwa akihubiri ikatoweka akilini mwake. Alikaa chini na kuanza kuomba zaburi iimbwe, na, baada ya wimbo, kwa utulivu kamili aliwaeleza wasikilizaji kilichotokea. Baada ya hapo alisimama, akataja kifungu kingine cha Maandiko, na kuhubiri bila maandalizi mahubiri yenye nguvu nyingi. Baada ya tukio hilo George aliandika sehemu ndogo tu za mahubiri yake, na hatimaye alitayarisha muhtasari tu wa kumwongoza katika kuhubiri.
Dkt. Matheson alianza uchungaji wake wa mwisho mwaka 1886 akiwa na umri wa miaka 44, alipokuwa mchungaji wa Kanisa kubwa la Parokia ya St. Bernard’s huko Edinburgh, ambapo mahubiri yake yenye ufasaha yalivutia daima umati mkubwa wa watu kwenye ibada. Hapa alikaa kwa miaka 13, kanisa lake likiongezeka kutoka washiriki 1,494 hadi 1,703 katika miaka mitano ya kwanza. Aliendelea kwa uaminifu kuhubiri injili na akajulikana kama mmoja wa wahubiri na wachungaji bora wa Scotland na aliheshimiwa sana huko Edinburgh alikoishi.
Kumekuwa na makisio mengi kuhusu chanzo cha dhiki ya akili iliyomsukuma mwandishi kuandika maneno haya. Simulizi linalojulikana sana, ingawa halijawahi kuthibitishwa, ni kwamba maneno haya yalitokana na jaribu kali alilokabili Matheson baada ya mchumba wake kumwacha muda mfupi kabla ya ndoa yao alipojua kwamba alikuwa karibu kupoteza kabisa uwezo wake wa kuona. Ingawa simulizi hili haliwezi kuthibitishwa kwa kumbukumbu, kuna vidokezo vingi muhimu katika wimbo huu wa ibada vinavyoonyesha moyo wenye huzuni, kama vile “mwenge unaopepea” na “mwale ulioazimwa” katika ubeti wa pili, kufuatilia “upinde wa mvua katikati ya mvua” katika ubeti wa tatu, pamoja na “msalaba” katika ubeti wa mwisho.
Kwa bahati nzuri, Dkt. Matheson alisimulia jinsi alivyoandika wimbo huu wa ibada:
“Wimbo wangu wa ibada ulitungwa katika nyumba ya mchungaji huko Innellan jioni ya Juni 6, 1882. Wakati huo nilikuwa peke yangu. Ilikuwa siku ya harusi ya dada yangu, na wanafamilia wengine walikuwa wakilala usiku huo huko Glasgow. Jambo fulani lilinitokea, ambalo nililijua mimi tu, na ambalo lilinisababishia mateso makali sana ya akili. Wimbo huo ulikuwa tunda la mateso hayo na ulikuwa kazi niliyoikamilisha kwa muda mfupi zaidi kuliko kazi nyingine yoyote maishani mwangu. Ulikuwa msukumo wa kweli; nilihisi kana kwamba sauti fulani ya ndani ilikuwa ikiniambia maneno ya kuandika badala ya mimi kuyatunga mwenyewe. Nina uhakika kabisa kwamba kazi yote ilikamilishwa kwa dakika tano na nina uhakika vilevile kwamba sikuwahi kuifanyia mabadiliko au masahihisho yoyote. Sina kipaji cha asili cha mdundo. Beti nyingine zote nilizowahi kuandika ni kazi zilizotungwa kwa juhudi; hii ilikuja kama alfajiri kutoka juu. Sijaweza kamwe kupata tena ari ileile katika kutunga beti.”
Wimbo huu wa ibada ulichapishwa kwa mara ya kwanza katika jarida la kila mwezi la Kanisa la Scotland, Life and Work, Januari 1883. Melodia ilitungwa mwaka mmoja baadaye na mpiga ogani maarufu wa Scotland wa wakati wake, Albert L. Peace, aliyeombwa kuandika melodia mahsusi kwa maneno ya Matheson.
Maelezo ya Peace mwenyewe kuhusu uandishi wa melodia hii nzuri ni kama ifuatavyo, “Baada ya kuyasoma kwa makini, niliandika muziki mara moja, na naweza kusema kwamba nilipomaliza melodia hiyo, wino wa noti ya kwanza ulikuwa bado haujakauka.” Asili ya jina la melodia, St. Margaret, haijulikani isipokuwa kwamba ni jina linaloheshimiwa sana Scotland, bila shaka kwa sababu ya Malkia Margaret wa Scotland aliyependwa sana.
Miaka ya mwisho ya maisha ya Matheson kuanzia umri wa miaka 57 hadi kifo chake akiwa na umri wa miaka 64 aliitumia kuandika baadhi ya maandiko bora zaidi ya kujenga maisha ya kiroho katika lugha ya Kiingereza, yakiwemo Moments on the Mount, Voice of the Spirit, na Rests by the River. Ingawa huu ndio wimbo wake pekee unaopatikana katika vitabu vingi vya nyimbo za ibada, aliandika pia nyimbo nyingine chache nzuri za ibada, zikiwemo “Nifanye Mateka, Bwana”, na “Ndipo Nitakapokuwa Huru.”
Maneno manne muhimu ya “Ee Upendo Usioniacha Niende” ni: upendo, mwanga, furaha, na msalaba. Maneno haya yameelezewa kuwa yanatoa uradhi kamili kwa mwamini yeyote ambaye maisha yake yamesalimishwa kabisa kwa mapenzi ya Mungu. Huenda ikachukua muda wote uliobaki wa maisha ya mtu kugundua kikamilifu maana ya maneno haya manne kwake binafsi.
Marejeo:
101 Hymn Stories
Treasury of Hymn Stories
Mwandishi -George Matheson, 1842 – 1906
Mtunzi wa melodia -Albert L. Peace, 1844 – 1912


