Ramona* alikuwa msichana mdogo mwenye shughuli nyingi na mchangamfu. Kama watoto wengine wa miaka minne, Ramona aliweza kufanya mambo mengi. Aliweza kuendesha baiskeli, kupanda mti, kuosha vyombo, kuandika jina lake, na kumpanda farasi wake mdogo peke yake. Mojawapo ya mambo aliyopenda sana Ramona kufanya ilikuwa kupanda farasi. Familia yao ilikuwa na farasi wawili na farasi mdogo mmoja. Jioni hizo zilikuwa za kufurahisha sana walipomfunga farasi wao mdogo, Tony, kwenye mkokoteni, kisha familia nzima ikapanda kwa zamu. Au Ramona na dada zake watatu walipopanda mgongoni mwa Tony na kwenda matembezini.
Ramona aliweza kufanya mambo mengi, lakini wakati mwingine alifikiri angeweza kufanya mengi zaidi ya yale aliyoweza kweli. Na wakati mwingine alifikiri alikuwa mkubwa zaidi kuliko alivyokuwa kweli.
Jioni moja nzuri ya kiangazi, wageni fulani walifika nyumbani kwa Ramona. Wageni walipokuja, kwa kawaida hiyo ilimaanisha wakati wa kufurahisha.
Jioni hiyo hasa, baada ya chakula cha jioni, ndugu zake wakubwa wa Ramona walikuwa wakipanda farasi pamoja na wageni. Ilionekana kufurahisha sana walipokuwa wakizunguka bwawa kwa mwendo wa kunyata na kupita kwenye nyasi. Ramona alitaka kupanda pia, lakini ilimbidi asubiri zamu yake. Alipokuwa akisubiri, alicheza kwenye nyasi pamoja na Clifford, mbwa. Muda si muda alichoka na mchezo huo, akaenda kuzunguka kwa baiskeli yake. Kisha wazo likamjia ghafla. Alikimbilia kwenye lango la kuingilia malishoni na kupanda juu yake. Alipenda kujifanya tumbili, akining’inia kwenye vyuma vya lango na kupanda juu na chini. Kisha akajaribu kusimama kwenye chuma kimoja kwa mizani na kuondoa mikono yake langoni. Ndugu zake pamoja na wageni wao walikuwa wakipanda farasi karibu na hapo. Ramona aliinua mikono juu, na huku akisawazisha mwili juu ya lango, akawapigia kelele wapandaji farasi, “Niangalieni! Niangalieni!” Alijihisi mkubwa sana kwa kusimama kwa mizani juu ya lango. Ghafla, mguu wake uliteleza, akaanguka chini kwenye vumbi. Alifumbua macho kwa mshangao na kuruka juu haraka, huku akipangusa vumbi kwenye gauni lake. Alitazama huku na huku kwa aibu, lakini ilionekana hakuna aliyegundua. Alipanda tena ubavuni mwa lango na kuanza kucheza. Ramona alizidi kukosa subira alipokuwa akisubiri zamu yake ya kupanda farasi. Ilionekana hakuna aliyekumbuka kwamba alitaka kupanda farasi. Alifikiri ingekuwa furaha kuona angeweza kusawazisha mwili juu kiasi gani kwenye lango, kwa hiyo alipanda juu kadiri alivyothubutu. Alitaka wengine waone jinsi alivyokuwa jasiri, kwa hiyo, huku akipunga mikono, akapaza sauti, “Jamani nyote! Niangalieni!” Lakini tena, mguu wake uliteleza kutoka kwenye lango. Hata hivyo, safari hii aliepuka kwa shida kuanguka chini. Baba yake Ramona alimwona na kumfuata. “Ramona,” alisema, “nataka usipande tena juu ya lango.”
Ramona alishuka na kujaribu kutafuta kitu kingine cha kufanya. Baada ya kucheza kwa muda, amri ya baba yake ya kutokupanda juu ya lango ilionekana kumponyoka akilini, akaanza tena kupanda lango. Kisha dada yake mkubwa, Elise, alimfuata na kumwambia kwa sauti ya chini, “Ramona, hupaswi kujionyesha mbele ya wageni wetu.” Ramona hakupenda ushauri huo. Uliingia sikio moja na kutoka lingine. Alijihakikishia kwamba hakuwa akijionyesha! Alikuwa tu… naam, alikuwa anacheza tu.
Alipanda juu kadiri alivyoweza, kisha tena akapunga mikono hewani, akipiga kelele, “Niangalieni, nyote!” Ghafla, kabla hajajua kilichokuwa kinatokea, alitua chini kwa kishindo na kuanza kulia kwa sauti kubwa. Bila shaka alihisi maumivu kiasi, lakini zaidi ya yote alishtuka na kuaibika.
Baba yake Ramona alimwendea na kumwinua, akihakikisha hakuwa ameumia vibaya, kisha akambeba hadi nyumbani. Kulikuwa bado na mwanga nje, na jioni ilikuwa bado changa, lakini alimpeleka ghorofani kitandani kwake.
Kabla ya kumlaza, alizungumza naye. Ramona alikuwa bado analia, na Baba alijaribu kumfuta machozi. “Ramona, sikiliza, unaweza kunyamaza kidogo? Unafikiri kwa nini ulianguka?” Alivuta kamasi na kuinua mabega. Baba akaendelea, “Kama ungenitii na kubaki mbali na lango kama nilivyokuambia, usingeanguka. Elise pia alikuambia uache kujionyesha, lakini hukumsikiliza. Je, unajua kwamba kujionyesha kwa kweli ni kiburi? Biblia inasema, Kiburi hutangulia uharibifu, na roho ya majivuno hutangulia anguko –Mithali 16:18.
Ramona aliitikia kwa kichwa. “Unajutia kuniasi, Ramona?” Baba akauliza. “Ndiyo, Baba, najutia,” akajibu huku akilia. Baba aliamua kwamba wakati huu adhabu yake iwe kuanguka na kulala mapema. Ramona angependelea kuchapwa viboko badala ya kulala mapema, jambo ambalo lilihuzunisha sana moyo wake mdogo. Lakini hilo lilikuwa jema kwake kwa sababu lilimfanya atubu.
Ramona hakusahau kamwe somo hilo, kwa sehemu kwa sababu ya kuanguka kwake, na kwa sehemu kwa sababu alipelekwa kulala mapema na akakosa furaha ya kupanda farasi. Hakuwa tu na kiburi kwa kujionyesha, bali pia alimwasi Baba kwa makusudi.
Elise alikuwa ametunga wimbo wa beti ambayo Baba alikuwa amemtajia Ramona. Tangu wakati huo, kila Ramona alipoimba wimbo huo, alikumbuka jinsi beti hiyo ilivyothibitika kuwa kweli kwake.
Huu hapa wimbo ambao Ramona aliimba:
*Majina katika makala hii yamebadilishwa

