Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote: kwa maana jambo hili humpendeza Bwana sana –Kol 3:20.
Miaka mingi iliyopita, kulikuwa na mvulana mmoja aliyeitwa Joey aliyeishi na baba na mama yake pembezoni mwa jiji. Siku moja baba yake Joey alimpa baiskeli mpya kabisa, nyekundu na nyeupe, ambayo alikuwa akiitamani kwa muda mrefu.
Karibu na nyumba yao kulikuwa na kilima kikubwa ambacho wavulana wakubwa wa jirani walifurahia kushukia kwa baiskeli zao. Baba yake Joey alimkataza kabisa kuendesha baiskeli pamoja na wavulana wakubwa kwenye kilima hicho, kwa kuwa kilikuwa hatari mno. Badala yake, aliruhusiwa tu kuendesha baiskeli kwenye njia nzuri, tambarare ya watembea kwa miguu, akipita nyumba nyingi, kupitia kichochoro kidogo, na hatimaye kurudi tena nyumbani kwake.
Siku na majuma yalivyopita, jambo hilo lilianza kupoteza msisimko wake. Aliwatazama kwa wivu wavulana wakubwa wakitembeza baiskeli zao kupanda kilima karibu moja kwa moja mbele ya nyumba yake. Wakiwa juu kabisa, waliruka juu ya baiskeli zao, na kwa shangwe wakashuka kwa kasi kwenye barabara ya lami, wakigeukia kwa wepesi barabara nyingine iliyoungana nayo chini ya kilima.
“Whee, tunakuja!” walipiga kelele walipokuwa wakipita kwa kasi, huku Joey akiendelea kukanyaga taratibu kuzunguka mtaa wake mdogo tena na tena.
“Njoo, Joey!” wavulana walipiga kelele. “Mbona hupandi pamoja nasi? Tazama tunavyofurahia! Unaogopa sana,” walimtania.
Joey aliona aibu mno kuwaambia kwamba baba yake alikuwa amemkataza kwa sababu alikuwa mdogo sana na huenda akaanguka kutoka kwenye baiskeli yake na kujiumiza. Wavulana wangemdhihaki zaidi tu, kwa hiyo alikaa kimya. Alitamani sana kupanda huko na kuwaonyesha rafiki zake kwamba hakuwa mwoga. Joey aliwaza, “Labda nikishuka kilima mara moja tu, baba yangu atatambua kwamba mimi si mdogo sana tena. Kisha Baba atajivunia na kuniruhusu kushuka kilima pamoja na wavulana wakubwa wakati wowote nitakapotaka. Lo, hilo lingefurahisha sana.” Wazo hilo tu lilifanya moyo wake upige kwa kasi kwa hamu ya kutarajia.
Joey hakuhitaji kusubiri muda mrefu kupata nafasi yake. Baba yake alipaswa kwenda kikazi kwa siku kadhaa. Joey alifikiri kwamba hii ingekuwa nafasi yake ya kumthibitishia baba yake kwamba alikuwa na uwezo wa kuendesha baiskeli pamoja na wavulana wakubwa. Akiwa na msisimko na hamu ya kutarajia, aliipandisha baiskeli yake kilimani. Alijihisi mtu mzima sana akiwa pamoja na wavulana wakubwa. Kwa hakika baba yake alikuwa amekosea! Sasa angemthibitishia kila mtu kwamba yeye ndiye aliyejua kuliko mtu mwingine yeyote kile alichoweza na asichoweza kufanya.
Kwa kujikimbiza na kuruka, alikuwa juu ya baiskeli yake. Baiskeli ilipozidi kwenda kasi, alizishika kwa nguvu zaidi ncha za usukani. Wakati huo, mmoja wa wavulana watundu, aliyekuwa akipanda kilima, alirusha jiwe kwenye tairi la Joey alipokuwa akipita kwa kasi. Joey aligeuka ghafla ili kulikwepa jiwe. Kabla hajatambua kilichokuwa kikitokea, alikuwa akiruka angani bila baiskeli yake. Alijiviringisha, akateleza na kujigonga, kabla ya kusimama kwa maumivu. Joey alikuwa amechafuka vibaya. Suruali na shati lake vilikuwa vimechanika. Alikuwa na michubuko na majeraha mikononi, magotini na usoni. Hakuwa tena akiwaza kuwa shujaa wa kile kilima kikubwa cha baiskeli. “Shujaa” wetu mdogo, aliyekuwa amenyenyekezwa, alirudishwa nyumbani kwa mama yake, ambaye kwa huruma na upendo alisafisha na kufunga majeraha yake.
Siku iliyofuata baba yake Joey alirudi nyumbani. Alipoona bendeji kwenye mwili wa mwanawe na baiskeli iliyoharibika, alikisia mara moja kilichotokea. Baiskeli ya Joey ilihifadhiwa kwa majuma kadhaa kama adhabu kwa kutotii kwake.
Joey aliketi kwenye ukingo wa barabara wavulana walipokuwa wakishuka kwa kasi kilima, kisha kuelekea barabara nyingine. Sasa Joey hakutaka tena kujificha na kuendesha baiskeli pamoja na wavulana wakubwa. Alikuwa amejifunza somo lake—kumtii baba yake sikuzote, hata alipofikiri kwamba yeye ndiye aliyejua zaidi. Alitambua kwamba baba yake hakuwa akijaribu kumnyang’anya furaha, bali alikuwa akijaribu kumlinda asiwe hatarini.
Joey alipopewa tena ruhusa ya kuendesha baiskeli yake, aliridhika kabisa kuendesha kwa amani kuzunguka mtaa wake mdogo wenye nyumba. Kuanzia wakati huo, angemtii baba yake, si katika mambo ya usalama tu, bali katika mambo yote.



