Kama wasichana, tumeumbwa tukiwa na hitaji la kutoshelezwa kihisia. Ingawa tamaa ya ndoa ni zawadi tuliyopewa na Mungu, Bwana pia ametupa neema tele ya kuishi kwa furaha bila mwenzi wa maisha, kwa miaka michache au mingi kadiri atakavyochagua. Katika kipindi hiki cha useja, Bwana anakusudia tupate uhuru wa kweli kwa kuwa Wake kabisa na kujitoa kwa upendo Wake usio na kifani. Miaka hii pia ina fursa ya pekee ya kukua sana kiroho na ya huduma.
Kwa sababu ya uwezo wake, kipindi hiki cha pekee maishani hulengwa na adui. Shetani akiweza kuifanya nafsi iwe mtumwa katika ujana wake, hufaulu kuiba zawadi nyingi za thamani ya milele: Ukristo wenye ushindi, ukaribu na Bwana, na huduma iliyotiwa mafuta. Miaka yetu ya ujana ni nyakati ambazo vita vingi muhimu hupiganwa na mienendo ya maisha huwekwa. Mara nyingi, vita na chaguo hizi hutengeneza maisha yetu sana hivi kwamba, kwa sababu yake, tunaishi miaka yetu ya utu uzima tukiwa utumwani au huru. Kama wanawake vijana wasioolewa, huenda vita vyetu vikubwa zaidi vikawa ni kudumisha moyo safi na kuzidhibiti hisia tulizopewa na Mungu. Mimi binafsi naamini kwamba tunachofanya—au, kwa usahihi zaidi, tulivyo—katika kipindi hiki cha pekee maishani ni muhimu mno kupita kiasi cha kupimika.
Kimsingi, naona kuna chaguo mbili. Utumwa au Uhuru. Utumwa wa hamu ya kutoshelezwa kimapenzi. Au, uhuru wa kuishi kwa furaha na kuridhika, na kumpenda Bwana kwa mioyo yetu yote.
Kwa sababu ya upendo na nguvu za Bwana wangu Yesu Kristo, nimejua uhuru huu mtamu. Umekuwa mzuri sana, wenye kuthawabisha na kuridhisha, kiasi kwamba siwezi kuizuia furaha yangu ndani yangu. Kweli nilizogundua katika safari yangu na Bwana zina uwezo mkubwa sana wa kubadilisha maisha kiasi kwamba siwezi kunyamaza.
Kwa hiyo, shauku yangu ya kuandika makala hii ni kwanza kabisa kuimba sifa za Mpendwa wangu. Amefunua upendo Wake kwangu na kuuteka moyo wangu. Ahadi Zake hazijashindwa.
Kisha, ninataka kushiriki maono yangu kuhusu uhuru wa kihisia. Mtu mmoja alisema kwa hekima: “Maono yasiyo na matendo ni ndoto. Matendo yasiyo na maono ni jinamizi. Lakini matendo yenye maono huleta uhalisi mzuri.” Mambo ninayoshiriki hapa ni baadhi ya maono yangu. Lakini kwangu ni zaidi ya hayo. Ni uhalisi mzuri; ni ushuhuda wangu. Kwa kuwa maono yanahitaji matendo ili yawe halisi, nimejumuisha baadhi ya mambo ya kivitendo tunayoweza kufanya sote ili kupata uhuru wa kihisia. Lakini, tuanze na mambo ya kwanza.
Tunahitaji Kuwa na Maono ya Uhuru Huo
Kwa wale mnaotembea katika uhuru, kweli nyingi ninazoshiriki hazitakuwa mpya. Tamaa yangu ni kuwatia moyo; msichoke kutenda mema! Mungu na aendelee kuwapa ushindi. Na tafadhali niombeeni mimi na uhusiano wangu na Mungu.
Lakini mzigo wangu hasa ni kwa wale wasiotembea katika ushindi. Baadhi yenu huenda mmefungwa na hisia zenu, na mnapigana vita mnayoshindwa. Mnatumaini kwamba mtaweza tu “kuvuka” miaka yenu ya useja. Mnahisi mzigo mzito, hamu kubwa isiyotimizwa. Hamjui upendo wa ajabu na wenye kuridhisha wa Yesu Kristo. Hamna furaha. Hamko huru. Ee, mnaposoma makala hii, imani na tumaini na viinuke mioyoni mwenu: mnaweza kuwekwa huru ili kumpenda Bwana Yesu kikamilifu! Mungu anataka kufanya kazi kubwa ndani yenu. . . naye anaweza! Mnaijue Kweli, Yesu Kristo, atakayewaweka huru. Na “Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.” (Yohana 8:36)
Hatua za Ushindi
Kama ilivyo katika kila sehemu ya mwenendo wa Kikristo, hatuwezi kushinda kwa nguvu zetu wenyewe. Juhudi zetu wenyewe zitakuwa bure na za kutukatisha tamaa. Tunahitaji neema ya Mungu, yaani, hamu na uwezo wa kufanya mapenzi ya Mungu. Tunapokuja mbele za Bwana kwa moyo uliovunjika, na kuutoa moyo wetu autunze, Yeye hukubali kujitoa kwetu. Njia pekee ya kuuhifadhi kwa kweli moyo wetu ukiwa safi kihisia ni kumkabidhi Bwana Yesu na kumtegemeza autunze. Akiwa Mchungaji Mwema, hapotezi wala kupoteza kile alichokabidhiwa. “. . . kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile.” (2 Timotheo 1:12)
Hatua moja tunayoweza kuchukua baada ya kujitoa kwa mara ya kwanza ni kuondoa kila fursa ya kuufuata mwili. “Wapenzi, nawasihi kama wageni na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho.” (1 Petro 2:11) Tayari ni vigumu vya kutosha kukabiliana na mapenzi na tamaa zetu wenyewe bila kuongeza majaribu yatokanayo na video, muziki na vitabu vya kilimwengu vinavyochochea hisia zetu! Mambo haya yanazuia kumpenda Yesu, huzaa kutoridhika, na kufifisha maono yetu ya kiroho. Tufanye jitihada za dhati kuondoa kila ushawishi unaodhuru maishani mwetu. Kujiondolea mizigo hii hutuwezesha kukimbia mashindano yetu.
Tunahitaji ushauri wenye hekima wa Baba yetu wa Mbinguni na wazazi wetu wa duniani ili kujua jinsi ya kuwa na mahusiano safi na vijana wa kiume. Mungu ametupa pia akili ya kawaida. Ikiwa tunatamani kweli kuweka mioyo yetu safi, hatutafanya mambo yanayochochea hisia zetu bila sababu. “ . . msitengeneze njia za kuufuata mwili, hata kuzitimiza tamaa zake.” (Warumi 13:14) Usafi wa moyo wetu ni wa thamani mno kiasi kwamba hatupaswi kuuhatarisha. Jiepusheni na hali zisizofaa. Hii inajumuisha kuanzisha urafiki wa pekee na vijana wengine wa kiume. Msichana aliyejitoa kabisa kwa Yesu anapaswa kuwatendea vijana wote wa kiume kwa namna ileile, bila kumwonyesha yeyote urafiki wa pekee. Ni jambo la kibiblia kuwatendea kama ndugu katika Bwana—lakini urafiki wa pekee na wa karibu (nje ya uhusiano mtakatifu wa uchumba) ni hatari na huleta mapambano yasiyo ya lazima.
Kukabiliana na Hisia
Jambo la msingi sana katika uhuru wa kihisia ni kumwachia Bwana mapenzi yote yanayoshindana na upendo wetu kwake. Pendo linaloshindana ni hamu ya kihisia au mvuto wa kimapenzi unaozuia utii na upendo kwa Yesu. Bila kujali hali yetu ya ndoa, Kristo anahitaji na anastahili nafasi ya kwanza mioyoni mwetu. Hata hivyo, uhuru wa kihisia haumaanishi kutokuwa na hamu ya kuolewa au kutowajali vijana wa kiume. Badala yake, ni uhuru wa kumpenda Bwana kwa moyo wote bila kukengeushwa. Kanuni hii inapatikana katika 1 Wakorintho 7:35.
Ni muhimu kuelewa kwamba kuvutiwa kihisia na vijana wa kiume si uovu. Wala si upendo; ni hisia tu ya kuwapenda. Zaidi ya hayo, si lazima tudharau hisia zetu, kana kwamba ni “kizuizi” au “tatizo.” Huwa tatizo tu zinapokuwa haziko mahali pake, zinapotutawala. Moyo wa Mungu ni kutumia mapambano ya usafi wa kihisia kutufanya tumtegemee Yeye kwa ukaribu. Tunapoitikia uongozi Wake wa Mchungaji, mambo yale yale yanayotufanya tupige magoti yatatumika kutufanya wanawake wa Mungu. Kisha tutaelewa jinsi hata pambano hili linavyoweza hatimaye kuleta mema katika maisha yetu yote (na hata milele).
Tunachofanya na hisia zetu huamua kama tutatembea katika uhuru au utumwa. Msichana akichagua kushikilia tamaa zake, kuzichochea na kuzificha, nafsi yake itakuwa mtumwa wa tamaa hizo. Jambo sahihi la kufanya tunapohisi kuvutwa kihisia kwa kijana fulani wa kiume ni kulikabidhi mara moja na kabisa kwa Bwana. Kwa maana “. . . walio wa Kristo wameusulubisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.” (Wagalatia 5:24)
Tunasoma katika Mwanzo kwamba Mungu, mpangaji wa ndoa wa milele, alimlaza Adamu usingizi alipokuwa akimwandalia mwenzi wa maisha, Hawa. Wakati wa Mungu ulipotimia kikamilifu, Adamu aliamka na kuwa mmoja na Hawa, “chaguo kamilifu” la Mungu. Simulizi hili la ndoa ya kwanza ni kwangu mfano wa kile Mungu anachotaka kufanya maishani mwetu. Mungu anaweza na yuko tayari kuleta pumziko la kweli mioyoni mwetu. Kwa upande wa hisia, “huwapa wapenzi wake usingizi.” (Zaburi 127:2) Hata hivyo, tunapopumzika mikononi mwa Baba, tunaweza kuwa na uhakika kwamba Yeye halali! Anatuandalia mwenzi kamilifu wa maisha, kama alivyomfanyia Adamu. Kwa kuzingatia kweli hizi, tafakari ahadi hizi nyororo za Mungu: “. . . akulindaye hatasinzia . . wala hatalala. . . BWANA ndiye mlinzi wako. . .” (Zaburi 121:3~5) Mungu “anapotutuamsha” wakati uliowekwa, ushuhuda wetu na uwe: “Mimi nalijilaza na kulala usingizi; nikaamka, kwa kuwa BWANA ndiye aliyeniinua.” (Zaburi 3:5)
Bwana ametupa pia wenye mamlaka wa kibinadamu, kwa kawaida wazazi wetu, ili watusaidie na kutuongoza katika masuala haya. Mungu anataka “tuwaweke” wazazi wetu mioyoni mwetu na tuwasiliane nao waziwazi kuhusu mapambano yetu ya kihisia. Uangalizi wao wa karibu ni baraka nzuri sana! Kuwajibika kwa uaminifu mbele ya baba na mama hutusaidia sana kupata uhuru wa kihisia. Hata udanganyifu kidogo utazuia sana maisha ya ushindi. Kadiri tunavyokuwa waaminifu na wazi zaidi kwa Mungu na wenye mamlaka wetu, ndivyo tutakavyofurahia uhuru zaidi. Mwanzoni, huenda ikaaibisha au kuwa vigumu kuzungumza na wazazi wako kuhusu wavulana na hamu ya kuolewa. Lakini kwangu, kadiri muda unavyopita inakuwa rahisi zaidi.
Wakati mwingine tunavutiwa zaidi kihisia na kijana wa kiume, hasa tunapokua na kuwa wanawake. Ninaposema “zaidi,” namaanisha kwamba si jambo la kupita tu. Huenda kweli unahisi ungependa kuolewa na mtu fulani, na “huwezi kuondoa” mvuto wa kihisia unaohisi. Kwa mambo mengi, majibu ni yale yale: mpe Mungu tamaa hiyo na uwe wazi na mwaminifu kwa wenye mamlaka. Lazima tuwe waangalifu hata zaidi kuulinda moyo na mwenendo wetu wa nje kuelekea mtu ambaye tunavutiwa naye hasa.
Lakini hilo halitoshi. Kujitiisha kwa Baba kwa kumtumaini kutatupa ushindi dhidi ya hisia zetu. Kujitiisha ni tendo la nia chini ya uongozi wa Roho wa Mungu. Huenda tusihisi mara moja kwamba kuna jambo limebadilika. Mara nyingi kuna pengo kati ya hisia zetu na nia yetu, lakini usichanganyikiwe na hilo.
Wakati wa mahitaji yetu, tunaweza kumwita Bwana na kumweleza mioyo yetu kwa uaminifu kamili. “Mungu, lazima nikuambie jinsi ninavyohisi sana kuhusu ‘fulani.’ Nahisi nataka uhusiano huu, Bwana. Lakini ninataka mapenzi yako zaidi. Kadiri ninavyojua, ninajisalimisha na kukukabidhi jambo hili kabisa. . . hata kama hutanipa kile ninachotamani. Nisaidie!” Naye atafanya hivyo. Humkaribia mwenye unyenyekevu na moyo uliovunjika, na kuujaza neema Yake mwenyewe.
Hali hii hunikumbusha kile Daudi alisema alipopewa bure vifaa vya kutoa dhabihu kwa Bwana: “Mfalme akasema . . . wala sitamtolea BWANA, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa za vitu ambavyo havikunigharimu chochote. . .” (2 Samweli 24:24) Mara nyingi dhabihu huwa na gharama kubwa kweli. Au angalau ndivyo inavyohisiwa.
Ninataka kuwa na mtazamo wa juu zaidi kuhusu kujisalimisha. Nataka kumfahamu Bwana alivyo na yale aliyonitendea kiasi kwamba niweze kumtolea dhabihu kwa hiari. . . hata iwe ngumu au yenye maumivu kiasi gani. Kutoamini kwa hofu, kufikiria mambo ya kidunia, au ukaidi hufanya kujisalimisha kuwa kugumu. Kujisalimisha huwa furaha tunapokuwa na imani thabiti, kama ya mtoto, katika wema kamili wa Baba na upendo Wake mkamilifu. Lakini, kama wimbo wa zamani unavyosema, “. . . hatuwezi kamwe kuthibitisha utamu wa upendo Wake mpaka tuweke vyote juu ya madhabahu; kwa maana kibali anachotuonyesha na furaha anayotujalia ni kwa wale watakaomwamini na kumtii.” (John H. Sammis, “Trust and Obey”)
Basi na tumtolee Bwana kwa furaha hata kile chenye gharama. Na tuwe na shauku ya mapenzi ya Mungu kutimizwa maishani mwetu. Na tujisalimishe kwake kwa furaha sasa badala ya kujisalimisha kwa huzuni baadaye. Siku moja katika Utukufu kila dhabihu itatoweka katika furaha ya Uwepo Wake.
Hamu Zetu Zinatimizwa
Kulinda mioyo yetu kwa bidii bila kutosheleza hitaji letu la upendo na usalama kutatuacha tupu na bila utulivu. Kwa sababu hiyo, uhuru wa kihisia haujakamilika bila kuwa na uhusiano wa karibu na Mwokozi. Kama Oswald Chambers alivyosema, “Moyo wa mwanadamu lazima uridhike, lakini kuna mmoja tu anayeweza kutosheleza shimo la mwisho lenye maumivu katika moyo wa mwanadamu, naye ni Bwana wetu Yesu Kristo.”
Watu wengi, hata Wakristo, hutafuta furaha bure kwa watu au vitu vya duniani. Katika jitihada za kupata utoshelevu, sisi wasichana hasa tuna mwelekeo wa kuona ndoa kuwa lengo kuu la maisha. Mawazo kama “Nikishaolewa ndipo nitakuwa na furaha kweli” yanaweza kuwa sehemu ya fikra zetu, hata bila kujua na kwa njia isiyo wazi.
Bila shaka, kuna furaha na utoshelevu mwingi katika ndoa—Mungu aliiweka iwe hivyo! Hata hivyo, hatari ya kuifanya ndoa kuwa sanamu ni kwamba tunamtazamia mwanadamu atupe kile ambacho Mungu pekee anaweza kufanya. Kosa hili litatufanya tukumbwe na kuvunjika moyo baadaye. Waume ni watu wa ajabu, lakini ni wanadamu. Hukosea, wana mipaka, na hawaishi milele. Nimeamini kwamba ni lazima kabisa tuimarishwe na kujengwa kwanza katika upendo wa Mungu. Zaidi ya hayo, tukiamini kwamba ndoa ndiyo chanzo cha utoshelevu wa msingi, tunakisia kimakosa kwamba wale ambao Mungu anawaita kwenye useja hawawezi kujua ukamilifu wa kweli, kwamba kwa namna fulani wanakosa furaha iliyo kuu kuliko zote. Jambo baya kuliko yote, tunasema kwamba Mungu hawezi kutimiza mahitaji yetu.
Lakini jambo hili si kweli hata kidogo. Akiwa Muumba wetu, Yesu Kristo anaweza kabisa kuuridhisha moyo wetu. Hii ni huduma aliyojiwekea mwenyewe, ingawa huongeza zawadi Zake za upendo wa kibinadamu. Ni mapenzi ya Baba yetu turidhike sasa, tukiwa na Yeye peke yake. Nina hakika kwamba hata marafiki zetu walioolewa na mama zetu wangekiri kwa urahisi kwamba Mungu ndiye msingi wa furaha ya kweli, na kwamba hakuna kitu wala mtu mwingine yeyote anayeweza kutosheleza hamu kuu kabisa za nafsi zetu.
Kwa kweli, ninahisi kwamba kupata utoshelevu katika Kristo ni mojawapo ya njia bora zaidi za kujiandaa kwa ndoa! Tumaini letu linapokuwa kwa Mungu, upendo na furaha yote katika ndoa vitakuwa kama krimu tamu juu ya keki. Ndoa yenye furaha kweli ni ile ambayo kila mwenzi anampenda Yesu kwanza na kuridhika ndani Yake. Lakini kwanza tunapaswa kufika mahali ambapo hatuhitaji mahaba. . . ambapo tumeridhika sana katika Mungu hivi kwamba chochote kingine anachotupa tunakipokea kwa shukrani iliyojaa, kama baraka ya ziada.
Tofauti na ndoa za duniani, uhusiano wetu na Yesu utaendelea milele. Kwa hiyo, inafaa kabisa kujitahidi kukuza uhusiano wetu Naye. Njia moja muhimu ya kuwa na ukaribu zaidi na Yesu ni kutumia muda pamoja Naye. Kuwasiliana kwa kusoma Neno la Mungu na kujibu kwa maombi ni njia za msingi za kuukaribia moyo Wake. Ukaribu na Bwana hutokea wenyewe na huendelea daima; si lazima uwe na mpangilio na urasmi kila wakati. Kutembea na Mungu ni zaidi ya wakati wa utulivu wa asubuhi. Anataka tuwe karibu kiasi cha kumweleza kila huzuni ya moyo na furaha tunapopitia maisha yetu ya kila siku.
Tangu nilipokuwa na umri wa miaka 15, nimeweka lengo la kupata ukaribu na utoshelevu katika Bwana Yesu Kristo. Nimeweka mahaba kando hadi wakati uliowekwa na Mungu na kuelekeza hisia zangu kwa Bwana. Kwa furaha ninaweza kushuhudia kwamba ametimiza na bado anatimiza ahadi aliyonipa: “Maana huishibisha nafsi yenye shauku, na nafsi yenye njaa huijaza mema.” (Zaburi 107:9)
Mojawapo ya baraka kuu za uhuru huu wa kihisia ni uthabiti na utoshelevu anaotupa Yesu. “Tumaini lililokawia huufanya moyo kuwa mgonjwa, bali tamaa itimizwapo ni mti wa uzima.” (Mithali 13:12) Kristo ndiye Tumaini letu ambalo haliwezi kuahirishwa. Hakuna haja ya mioyo yetu kuugua tunapokuwa tunampenda Yesu! Si lazima kabisa tupitie kupanda na kushuka kwa hisia kwa kiwango kikubwa na hamu kuu zisizotimizwa. Bila shaka, huenda kukawa na siku tunazohisi vibaya na tunazopambana zaidi. Lakini kwa jumla, kunaweza kuwa na uthabiti na utoshelevu katika Kristo unaotuwezesha kuvuka miaka ya useja kwa ushindi na furaha.
Sisemi jambo ambalo ni ndoto nzuri tu: linaweza kuwa uhalisi kwa kila mmoja wetu! Unaweza kuwa huru kadiri unavyotaka! Unapata Kristo kwa kiasi unachotaka! Yeye huwathawabisha wale wanaomtafuta kwa bidii. Nina uhakika kabisa katika uwezo Wake: hana upungufu wa kile kinachohitajika ili kutimiza mahitaji yetu ya ndani kabisa!
Wapenzi Wenye Bidii wa Yesu Kristo
Amy Carmichael ni mtu ambaye maisha yake nayaheshimu sana kwa sababu ya ukaribu wake na Yesu. Kujitoa kwake kwa dhati kwa Kristo na huduma kulimzuia asiangukie katika kutoridhika. Lakini kulikuwa na wakati maalumu maishani mwake ambapo Mungu alisema naye kwa namna ya pekee na kumpa nguvu za kuishi maisha ya useja kwa ajili ya Bwana. Hivi ndivyo alivyomshirikisha mmoja wa watu wa familia yake ya Dohnavur: “Siku kama ya leo miaka mingi iliyopita, nilikwenda peke yangu kwenye pango katika mlima uitwao Arima, huko Japani. Nilikuwa na hofu nyingi kuhusu wakati ujao. Ndiyo maana nilienda huko. Nilitaka kuwa peke yangu na Mungu. “Shetani aliendelea kunong’ona, ‘Ni sawa sasa, lakini itakuwaje baadaye? Utakuwa mpweke sana.’ Naye alichora picha za upweke. Bado ninaziona.
“Kisha nilimgeukia Mungu wangu kwa kukata tamaa, nikasema, ‘Bwana, nifanye nini? Ninawezaje kuendelea hadi mwisho?’ Naye akasema, ‘Hakuna hata mmoja wa wale wanaonitumaini atakayekuwa ukiwa.’ (Zaburi 34:22)
“Neno hilo limekuwa pamoja nami tangu wakati huo, nami nakupa sasa. Limetimizwa kwangu. Litatimizwa kwako. Ishi tu kwa ajili Yake aliyekukomboa na umtumaini akutunze, naye atafanya hivyo.”” (Candles in the Dark, na Amy Carmichael, uk. 17)
Kusoma ushuhuda wake karibu hunifanya nihisi mtetemeko ninapotafakari maana ya ajabu ya alichoshiriki: “. . . Limetimizwa kwangu. Litatimizwa kwako.” Nasi litatimizwa kwetu, ikiwa tutathubutu pia kumwamini Mungu atimize ahadi Zake. Je, tunamtumaini Kristo atupende kwa ukaribu . . . atutegemeze . . . aturidhishe? Kwa kadiri ya imani yetu, na iwe kwetu.
Amy Carmichael ni mfano wa kile ninachokiita “mpenzi” wa Yesu. Alimpenda kwa makusudi, akitamani ukaribu mtamu. Wakati mmoja aliandika maneno yanayofichua hamu za moyo wake: “Ninaamini na kutumaini kwamba utazidi kumpenda Mwokozi aliyesulubiwa. Anataka wapenzi. Lo, upendo wa wengi wanaojiita kwa jina Lake una uvuguvugu kiasi gani. Upendo wetu wenyewe—wangu mwenyewe—una uvuguvugu kiasi gani ukilinganishwa na moto wa lava wa upendo Wake wa milele. Ninaomba uwe mpenzi mwenye bidii, aina ya mpenzi anayewasha wengine moto.” (Amy Carmichael, Candles in the Dark, uk. 107)
Tamaa kuu ya moyo wangu ni kuwa mmoja wa wapenzi wa kweli wa Bwana, kama Mtume Yohana na kama Maria, aliyeketi miguuni pake. Sitaki tu kuwa karibu Naye, bali nataka maisha yangu yawachochee wengine wamfuate. Ningependa kuwa mpenzi mwenye bidii wa aina hiyo, anayewasha wengine moto. Ninamwamini Bwana anifanye hivyo na kuendeleza kazi aliyoianza. Natumaini kwamba Bwana ataniambia atakaponiita Nyumbani: “upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu.” (2 Samweli 1:26)
Kwa Kumalizia . . .
Inasisimua kufikiria kuhusu usafi na uchangamfu wa mwanamke kijana aliye huru kihisia. Akimpenda Yesu na kuridhika ndani Yake, furaha yake yenye kung’aa huambukiza wengine. Amebeba harufu nzuri ya Kristo inayowavuta wengine wamtafute. Lakini tunajua kwamba ushuhuda huo mzuri haupatikani kwa kutamani tu. Huanza kwa kuchagua kutembea katika uhuru, kusalimisha tamaa za ndoa, kumpenda Bwana kwa mioyo yetu yote, na kuamini kwamba Kristo anaweza kabisa kutimiza mahitaji yetu.
Ninajiuliza ni wangapi kati yenu watakaofanya chaguo hizi. Je, utachagua uhuru wa kihisia? Ni nani kati yenu ambaye mwaka mmoja kutoka sasa atakuwa na ushuhuda wa kuwa mpenzi wa kweli wa Yesu? Je, utajua utimilifu wa furaha inayopatikana katika Uwepo Wake mtamu? Ni wangapi kati yenu mtakaomsikia akisema, “upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu?” Chaguo ni lako. Ni wazi kwamba chaguo hili lina athari isiyokadirika kwa maisha ya watu wengine zaidi ya yako mwenyewe. Hivi karibuni au baadaye, ulimwengu unaokuzunguka utajua uamuzi uliofanya.
Natumaini na kuomba kwamba utamfuata Mchungaji hadi “mahali pa juu” pa upendo Wake. . . hadi maisha tele ya furaha na uhuru. Upendo Wake ni kama bahari isiyokwisha, na ahadi Zake ni za hakika vya kutosha kutubeba katika safari yetu. Tunachohitaji ni kuchukua siku moja baada ya nyingine. Tukiwa na uhakika wa utulivu katika Yule anayetuelekeza . . . na tufurahie safari.



